KATIBU Mkuu wizara ya mambo ya ndani
ya nchi Mbarak Abdulwakil amesema, uhusiano kati ya TUGHE na mwajiri
usipofahamika vyema kwa pande zote mbili unaweza kuchukuliwa kama uhusiano wa
mashaka au wa kutoaminiana wakati haipaswi kuwa hivyo.
Abdulwakil aliyasema hayo jana
wakati akizindua Baraza dogo la wafanyakazi Idara ya Uhamiaji lililofanyika
mjini hapa ambapo alisema kuwa ili kujenga uhusiano mzuri baina yao na TUGHE
inapaswa viongozi wa idara kujitoa kuongea na uongozi huo mara unapofika kwa
ajili ya mazungumza ili kuweza kuleta usawa na usahihi katika masuala ya kazi.
Alisema kuwa wakati uongozi wa TUGHE
ukiendelea kutetea maslahi ya wafanyakazi lakini pia utakuwa mstari wa mbele
katika kujenga na kusimamia nidhamu na uwajibikaji wa watumishi katika kazi ili
kuongeza ufanisi na tija kwenye kazi husika.
Katibu mkuu huyo alisema, ifahamike
kwamba haki inatakiwa kwenda sanjari na wajibu na kwamba kama mfanyakazi
atatekeleza wajibu wake ipasavyo anaamini hata haki yake ataipata kwa wakati
tofauti na mfanyakazi ambaye hawajibiki ipasavyo, mtoro, mlevi, mtovu wa
nidhamu ambaye hata TUGHE haitaweza kumtetea mfanyakazi wa aina hiyo.
Hivyo alisema kuwepo kwa mipango
inayozingatia mahitaji na uwezo wa Idara bila malumbano, bali kwa staha,
ustahimilivu, weledi na kwa kuzingatia sheria na kanuni zinazotawala mabaraza
ya wafanyakazi mahala pa kazi sambamba na viongozi na wajumbe wa baraza hilo
kufahamu na kutumia sheria, kanuni na taratibu zinazotawala vikao vya baraza
katika kutekeleza majukumu yao .
Naye Kamishna mkuu wa Idara ya
uhamiaji Magnus Ulungi alisema, sheria za kazi na mikataba mahala pa kazi
zinaelekeza kuwa mahali ambapo kuna watumishi wanaofikia kumi na kuendelea
pawepo na Chama Cha wafanyakazi na mabaraza ya wafanyakazi kwa lengo la
kusimamia maslahi ya wafanyakazi pamoja na mustakabali mzima wa maendeleo ya
Taasisi husika.
0 comments:
Post a Comment