Wizara ya kilimo chakula
na ushirika imelenga kuendeleza skimu za umwagiliaji 78 Tanzania ili kutekeleza
mfumo wa Tekeleza sasa kwa matokeo makubwa (BRN) ikiwa ni muendelezo wa
kuboresha mpango wa kilimo kwanza hapa nchini.
Akizungumza kwenye mafunzo kuhusu
mfumo wa matokeo makubwa sasa (BRN) kwa watendaji wa sekta ya kilimo Mhandisi
wa umwagiliaji kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa wa Morogoro Evodius Lulazi alisema,
mfumo huo umeweza kuingiza skimu 23 za umwagiliaji kutoka katika wilaya 4 za
mkoa wa Morogoro.
Alizitaja wilaya hizo kuwa ni pamoja
na Kilombero 9, Kilosa 7, Morogoro vijijini 4 na Mvomero 3 na kwamba wilaya
hizo ikiwemo wilaya ya Ulanga zitatumika kama wilaya za mfano za utekelezaji wa
mfumo huo kimkoa ambazo pia zitawanufaisha wakulima wa maeneo husika na maeneo
jirani.
Alisema, kufuatia Serikali kutenga
mazao matatu yakiwemo mahindi, mpunga na miwa katika kutekeleza mfumo huo
wanatarajia kufungua hekari 25 za uwekezaji wa mashamba ya miwa wilayani
Morogoro ili kufanya uzalishaji wa sukari kuwa mkubwa hapa nchini na kuongeza
pato na kukuza uchumi wa Taifa.
Akifungua Mafunzo hayo Katibu Tawala
Msaidizi (Uchumi) Lameck Loah alisema, chimbuko la mfumo huo limekuja baada ya
Serikali kuchukua maamuzi ya kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka
2025 na kubaini uwepo wa kasi ndogo ya utekelezaji wa miradi, programu na
mikakati ya maendeleo na kusababisha Serikali kurejesha utaratibu wa maendeleo
ya muda wa kati yaani miaka mitano.
Alisema, mahitaji ya Dira
yalionyesha kuwa kuna hitaji la kuongeza kasi ya utekelezaji wa mipango ya
maendeleo na kuamua kuasili mfumo unaotumika nchi za Malaysia , Indonesia na
Korea Kusini wenye lengo la kuchagua na kutekeleza vipaumbele vichache vyenye
kuleta matokeo makubwa naya haraka.
Aidha Noah alisema kuwa pia mfumo
huo una nidhamu ya hali ya juu katika utekelezaji na kuwa na vigezo bayana vya
kupima kiwango cha mafanikio katika utekelezaji ili kuimarisha uwajibikaji wa
viongozi na watekelezaji.
Tayari wakurugenzi wa Halmashauri
zote nchini na washauri wa kilimo katika mikoa wameshapatiwa mafunzo ya namna
ya kukabiliana na mfumo huo ili kupiga hatua katika malengo ya kilimo kwanza
ndani ya mfumo huo wa (Big Result Now, (BRN) ambao utekelezaji wake kimfumo
unaisha mwaka 2015.
0 comments:
Post a Comment