JUMUIYA ya Umoja wa vijana mkoa wa Morogoro  UVCCM imepongeza kamati kuu ya chama cha Mapinduzi CCM kumpitisha Sixtus Mapunda kuwa katibu mkuu wa jumuiya hiyo. 
 
 
Akiongea na waandishi wa habari jana ofisini kwake mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Morogoro Harriet Sutta alisema kuwa CCM imewatenda haki vijana kwa kumchagua Mapunda kuwa katibu wao na kuahidi kumuunga mkono katika utendaji wake wa kazi za kila siku.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa baada ya kamati kuu kumpitisha katibu baraza kuu la UVCCM taifa nalo lilimpitisha  hali inayoonyesha dhairi kuwa katibu huyo ni chagua la UVCCM na kwamba hawakufanya makosa.
‘’ Tunapongeza Kamati kuu ya CCM kumpitisha Mapunda kwani ni kiongozi ambaye ametokana na umoja wa vijana , hivyo anaujua kwa kina umoja huu na hivyo itakuwa rahisi kutatua kero zetu na kutekeleza majukumu ya UVCCM bila shaka yeyote’’ Alisema
Alisema kuwa UVCCM mkoa wa Morogoro wanaandaa mapokezi makubwa ya kumpongeza kiongozi huyo ambayo yataambatana na shughuli mbalimbali zikiwemo za kufungua mashina sambamba na kuingiza vijana mkoani hapa.
Nao makada wa mkoa wa Morogoro wakiongea kwa nyakati tofauti Salumu Mkolwe ambaye ni mwenyekiti wa UVCCm Morogoro mjini, Samuel Msuya  diwani kijana wa Mbuyuni walisema kuwa  wamepokea kwa furaha uteuzi huo na kwamba nafasi hiyo haikupotea bali imefika mahali pale.
Mkolwe alisema kuwa Mapunda alikuwa kiongozi ambaye anapenda kushirikisha vijana katika shughuli mbalimbali za chama wakati alipokuwa akikaimu nafasi ya katibu wa CCM mkoa wa Morogoro hivyo kwa nafasi hiyo anaamini inamfaa.
‘’ Ni kijana mwenzetu aliyetokea katika chimbuko la vijana, hata wakati alipokuwa katibu wa mkoa wa Morogoro tuliona juhudi zake na mchango wake kwa vijana, aliwapenda na kuwashirikisha vijana, hatuna budi kumuunga mkono katika shughuli zake’’ Alisema Msuya.
Mwisho