WANAFUNZI wawili wa kidato cha
kwanza katika shule ya sekondari matombo katika wilaya ya Morogoro
wamejeruhiwa, na wengine watatu kunusurika, baada ya kulipukiwa na kitu
kinachosadikiwa kuwa ni bomu, wakati wakitoka shuleni.
Wanafunzi hao waliojeruhiwa katika
sehemu mbalimbali za miili yao ni Lucien Juma (14) na Anthonia Charles (15),
wakazi wa kijiji cha Konde, Tarafa ya Matombo wilayani Morogoro.
Lucien aliyelazwa katika hospitali
ya rufaa ya mkoa wa Morogoro kwa matibabu, aliwaambia waandishi wa habari
hospitalini hapo kuwa walipatwa na tukio hilo wakati wakitokea shuleni,ambapo
njiani walikutana na kitu mfano wa balbu ya tochi ambacho hata asubuhi
wakati wa kwenda shule walikiona na kukipuuza.
Alisema wakiwa kundi la watu
watano, njiani kutoka shuleni,walikikuta tena kitu hicho, ambapo mmoja wa
wanafunzi aliyekuwa akila muwa, alikirushia kitu hicho ganda la muwa na
kulipuka na kutoa mshindo mkubwa uliosikika hadi maeneo ya mbali.
Daktari Francis Semwene, anayemtibu
Lucien katika wadi namba moja alikolazwa, alisema majeruhi huyo anaendelea
vizuri, na amepata majeraha katika sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwemo
sehemu za siri, kwenye paja na sehemu ya nyonga na kwamba katika maeneo hayo
walifanikiwa kutoa vitu mfano wa vyuma vidogo vidogo.
Naye babu wa mwanafunzi Lusiani,
Ekaristi Martini, mkazi wa kijiji cha Konde, alisema walipata taarifa za tukio
hilo wakiwa shamba wanaendelea na kilimo, na baada ya kufika eneo la tukio
walikuta wasamaria wema wamewasaidia watoto hao na kuwapeleka hospitali ya
misheni ya matombo, ambapo walipatiwa huduma ya kwanza na kupewa rufaa kuja
hospitali hiyo ya mkoa kwa matibabu zaidi.
Kaimu kamanda wa Polisi mkoa wa
Morogoro John Laswai, alithibitisha kujeruhiwa kwa wanafunzi hao, ambapo
majeruhi Anthonia ametibiwa na kuruhusiwa na kwamba polisi wanaendelea na
uchunguzi zaidi kubaini kitu kilichowajeruhi wanafunzi hao, ambacho kilitoa
mshindo mkubwa na mtawanyiko wa vyuma, kama kilikuwa ni bomu ama vinginevyo.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment