MAKALA maalumu ya migogoro ya ardhi wilayani Mvomero.
WILAYA ya Mvomero ni miongoni mwa
wilaya zinazokabiliwa na migogoro ya wakulima na wafugaji iliyoduma kwa muda
mrefu hapa nchini.
Migogoro hiyo imekuwa ikisababisha
maafa ikiwemo mali kuharibiwa na wakati mwingine vifo na baadhi ya wananchi
kujeruhiwa vibaya.
Kwa Mvomero changamoto hiyo
inasababishwa na ufinyu wa eneo la ardhi na mgawanyo wa matumizi bora ya ardhi
kati ya wakulima na wafugaji.
Wilaya hiyo miongoni mwa wilaya sita
za mkoa wa Morogoro, wakazi wake kwa asilimia kubwa wanajishughulisha na
kilimo.Ina ukubwa wa kilometa za mraba 7,325 ambalo ni sawa na Hekta 732,500.
Kwa mujibu wa takwimu za sensa ya
watu na makazi ya mwaka 2012 wilaya hiyo ina wakazi wapatao 312,109 kati yao
wanaume ni 154,843 na wanawake ni 157,266.
Kulingana na takwimu za sensa,
wilaya hiyo ina wafugaji wapatao 18,749 wanaomiliki ng’ombe wa asili
138,396 na ng’ombe wa maziwa 10,744.
Mifugo mingine ni mbuzi 74,547,
kondoo 20,459, Wakati eneo linalofaa kwa ufugaji ni hekta 266,400 sawa na
ekari 676,656.
Hata hivyo kwa mujibu wa wataalamu
eneo ng’ombe mmoja huitaji ekari 10 za malisho kwa mwaka na kwamba eneo hili
linatosha ng’ombe 67,666 ambapo mbuzi kondoo hawatakuwa na eneo la malisho.
Kwa upande wa kilimo takwimu zinaonyesha
licha ya asilimia 82 ya wakazi kufanya shughuli za kilimo lakini asilimia saba
hufanya biashara na asilimia moja ufugaji huku wengine asilimia 10
wakifanya kazi mbalimbali.
Hata hivyo shughuli za kilimo
zinafanywa katika eneo dogo la wilaya hiyo. Kati ya Kilometa za mraba 549,379
zinazofaa kwa kilimo , zinazotumika ni hekta 247, 219 ambazo ni sawa na
asilimia 45.
Pia eneo linalofaa kwa kilimo ni
hekta ambapo eneo linalolimwa ni wastani wa hekta ambazo ni sawa na asilimia 45
ya eneo lote.
Hata hivyo kumekuwa na idadi kubwa
ya mifugo na kwamba imekuwa ikibadilika mara kwa mara kutokana na ufugaji
wa kuhamahama hasa wakati wa kiangazi ambapo wafugaji huamisha mifugo
kufuata maji na malisho.
Tatizo la ufinyu wa ardhi linatajwa
na Mkuu wa wilaya ya Mvomero, Antoni Mtaka kuwa ni tatizo linalosababisha
migogoro hiyo.
Mbali na uhaba wa ardhi pia kuna
tatizo la kutozingatia mgawanyo wa ardhi inayotengwa kwa kazi fulani.
Ni kutokana na migogoro hiyo iliyoduma
kwa muda mrefu Mtaka alisema wameanzisha kauli mbiu isemayo “
Ardhi haiongezeki watumiaji wa ardhi
wanaongezeka’’.
Mtaka alisema kutokana na migogoro
hiyo inayotokana na ufinyu wa ardhi, wilaya imeandika barua kwa Mkuu wa Mkoa wa
Morogoro, Joel Bendera, kuomba kufutwa kwa mashamba pori yapatayo 50
yaliyotelekezwa ili yagawiwe kwa wananchi.
‘’ Endapo mashamba hayo yatarudishwa
na kugawiwa kwa wananchi itasaidia kupunguza migogoro ambayo chanzo chake
kikubwa ni kukosekana kwa ardhi na hivyo wakulima na wafugaji kugombea ardhi
hiyo finyu’’ anafafanua .
Kutokana na hilo Mtaka alisema
Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi imeunda kikosi kazi ambacho kinasaidia
upimaji wa ardhi katika wilaya hiyo ili kuweza kubaini mipaka ya vijiji vyote
115 vilivyopo katika kata 23 za tafara 4 za wilaya hiyo.
Kwa mujibu wa sheria ya ardhi
kifungu cha 3, ardhi yote ya Tanzania ni mali ya umma na kwamba
Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ndiye mwenye mamlaka kwa niaba ya Watanzania
wote.
Na kulingana na sheria hiyo Rais
ndiye mwenye uwezo wa kufuta umiliki wa ardhi pale anapoona inafaa kufanya
hivyo kwa manufaa ya umma.
Hivi karibuni mapema mwezi
Januari Naibu Waziri wa Ardhi, George Simbachawene aliahidi mbele ya viongozi
wa wilaya hiyo kuwa endapo migogoro hiyo haitapata suluhu katika kipindi hiki
wizara yake ilivyoounda kikosi kazi hicho cha upimaji wa ardhi yuko tayari
kujiuzuru.
‘’ Kama migogoro hii ya ardhi
haitafikia tamati, niko tayari kujiuzuru nafasi yangu hii, siko tayari
kuona migogoro hii ikiendelea na kusababisha uvunjifu wa amani, watu kupoteza
mali zao na hata maisha,” ni kauli ya Simbachawene.
Naye Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi, Kaika Saning’o Telele, Februari 21 alipotembelea wilaya ya
Mvomero alisema ‘’ tayari tuna migogoro ya ardhi ya kutosha hatuitaji migogoro
mingine,’’ alisema.
Kwa mujibu mara nyingi migogoro hiyo
inatokana na ugawaji wa ardhi usiozingatia matumizi bora ya ardhi na na kwamba
mara nyingi wamekuwa wakipewa wawekezaji maeneo hata ya wafugaji na hivyo
wafugaji kukosa maeneo na kuanza kugombania kwa na wakulima.
‘’ Maeneo ya wafugaji anapewa
mwekezaji anajenga hotel wafugaji wanaogea na mara nyingine hata kuingia katika
hifadhi na hivyo kusababisha migogoro hiyo’’ alisema.
Musa Rajabu mkazi wa Turiani
wilayani Mvomero alisema kuwa imefika wakati sasa kuangalia uwezekano wa
kutengua hatimiliki za mashamba pori na kuwagawia wananchi kwa kuwatenganisha
wakulima na mafugaji ili kuepusha migogoro.
‘’ Ili migogoro iweze kupata suluhu
hakuna budi kwa serikali kuangalia uwezekano wa kutwaa mashamba hayo
yasiotumika kwa miaka mingi sasa ili kuwapatia wananchi kuweza kuyatumia kwa
shughuli za kibinadamu,’’ alisema.
Rehema Juma mkazi wa kijiji
cha Mkindo wilayani humo alisema kuwa migogoro hiyo pamoja na kuwepo kwa ufunyu
wa ardhi lakini pia umekuwa ukichangiwa kwa kiasi kikubwa na baadhi ya
wenyeviri wa vitongoji na vijiji kuwakaribisha wafugaji wageni kinyemela .
Alisema kuwa pia kumekuwa na tabia
kwa wafugaji wazawa kuwakaribisha wafugaji wavamizi kimya kimya na kwamba
wanapokuja wanakuja bila mifugo na kusoma ramani kisha kufuta mifugo yao na
hali hiyo imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa migogoro hiyo.
Kwa upande wake Mbunge wa
Morogoro Kusini, ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM mkoa wa Morogoro,
Inocent Kalogiries katika kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa kilichofanyika
mapema mwezi Januari alisema kuwa mbali na kuomba mashamba pori hayo kufutiwa
umiliki wake lakini pia mkoa wa Morogoro kwa sasa hawahitaji wafugaji.
‘’Mkoa wa Morogoro ni mkoa wa kilimo
sasa hawa wafugaji wanatoka wapi, kwanini tunawafumbia macho, ni lazima
tuchukue hatua,’’ Alisema.
Naye Mkurugenzi wa Kituo cha
Msaada wa Sheria, Frola Masoy alisema wilaya ya Mvomero ni moja ya wilaya
ambayo walifanyia utafiti juu ya migogoro hiyo na kuamua kutoa elimu kwa
wananchi wake kwaajili ya kumiliki ardhi.
Alisema wananchi hao walifundishwa
jinsi ya kujiandisha na kuomba hatimiliki za kimila ili kuweza kumiliki
kihalali na kuondokana na migogoro isiokuwa ya lazima na kwamba kuweza
kuzitumia katika kupata mikopo kwa lengo la kujikwamua kiuchumi.
‘’ Tumewafundisha wajue kuwa
ardhi inaweza kumilikiwa kimila na badae kuomba hatimiliki za kudumu, sambamba
na umilikaji wa pamoja kwa maana ya mume na mke,’’ Alisema.
Alisema kuwa umiliki wa pamoja wa
ardhi umekuwa ukisaidia pia kuondokana na migogoro ya ardhi katika
familia na kwamba mara nyingi mwanaume anapomiliki ardhi peke yao imekuwa
ikisababisha migogoro mingi pale anapofariki dunia na ndugu wa mwanaume
kuamua kutwaa mali za ndugu yao.
Viongozi wa wilaya hiyo akiwemo
mkurugenzi, wakuu wa idara wa halimashauri , na mwenyekiti wa halmashauri hiyo
, viongozi wa chama cha Mapinduzi wilaya hiyo, kamati ya ulinzi na usalama ya
wilaya walifanya ziara ambapo walikutana na wenyeviti wa vitongoji 640 wenyeviti
na watendaji wa vijiji 115, watendaji wa kata 23 pamoja na madiwani wote na
maafisa tarafa 4 kwa lengo la kutoa maelekezo juu ya kutatua migogoro hiyo.
Katika maelekezo hayo wananchi
walitakiwa kutouza maeneo yao hovyo pamoja na kutoingiza wafugaji
kiholela na kujenga tabia ya kuwa na vikao vya ujirani mwema mara kwa
mara ili kutatua migogoro inapokuwa katika hatua za awali badala ya
kusubiri inapokuwa katika hatua mbaya hali inayofanya kutumia nguvu kubwa
kutatua.
Pia viongozi hao waliwataka wafugaji
wavamizi kuondoka nje ya wilaya hiyo na kurudi maeneo waliotoka ili kupunguza
wingi wa mifugo na uharibifu wa mashamba wa makusudi kutokana na
utafiti uliobaini kuwa wafugaji hao wavamizi huvamia mashamba ya wakulima
nyakati za usiku na kulisha mifugo yao katika mashamba hayo.
Pamoja na mambo mengine uongozi huo
ulisitisha shughuli zote za ulinzi wa jadi na badala yake shughuli zote za
ulinzi zitafanywa na jeshi la polisi, hatua hiyo ilikuja baada ya kuwepo kwa
vijana waliounda kikundi cha asili kijulikanacho kama Mwano ambacho kilitoka
katika kundi la wakulima kilichokuwa na kazi ya kukamata ng’ombe na
kuwashikilia kisha kutoza fedha kama fidia kwa mfugaji atakayeonekana kuingiza
ngombe wake katika mashamba ya wakulima.
Zoezi hilo la kikundi hicho
lilichangia kwa kiasi kikubwa mapigano baina ya wakulima na wafugaji hasa pale
wanapokamata ng’ombe na kutoza faini hata kama mfugaji akiamua kufanya makubaliano
na mkulima mwenyewe na hivyo kusababisha wakulima nao kutumia silaha za
moto kuwadhibiti kundi hilo ambalo mara zote limekuwa likitumia silaha za jadi.
Kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro
Faustine Shilogile alisema kuwa kamati ya ulinzi na usalama iliamua kusitisha
shughuli hizo za ulinzi kwa kundi hilo kutokana na kutokea madhara makubwa
Novemba mwaka jana ambapo vijana hao walizuia ng’ombe wa 200
wanaomilikiwa na Semwako Matunda baada ya ng’ombe zake kuingia katika mashamba
ya wakulima 4 katika kijiji cha Hembeti wilayani humo.
Kamanda huyo anaelezea tukio hilo
kuwa wakulima hao walikamata ng’ombe hao na kupeleka katika ofisi ya
kijiji ili kupzta muafaka wa uharibifu huo katika mashamba yao na kwamba
ofisi ya kijiji ilimwita mfugaji huyo ili kupata muafaka wa tatizo hilo
ambapo wakulima walimtaka mfugaji huyo kulipa kiasi cha shilingi milioni
3 kitu ambacho mfugaji huyo hakuridhia na kuwataka wakulima hao kupeleka
suala hilo polisi.
Alisema kuwa kundi hilo la mwano
ambalo tayari lilishapigwa marufuku shughuli hizo walikataa na kuendelea
kuwashikilia ng’ombe hao ambapo ilipofika Novemba 5 mmiliki wa ng’ombe
huyo na vijana kadhaa wa Morani walifika katikan ofisi hiyo ya kijiji
ambapo ng’ombe hao walikuwa chini ya ulinzi na kuwataka kutoa mifugo hiyo
kitendo ambacho hakikufikiwa muafaka na kundi hilo na hivyo kuanza
mapigano baina ya pande hizo mbili.
Alisema kuwa madhara yaliotokea
katika mapigano hayo watu sita walifariki dunia huku wengine 35
kujeruhiwa sambamba na wananchi wa vijiji vya Hembeti, Dihombo,
Msufini na Mkindo walifanyiwa uharibifu wa mali zao kwa kuchomewa nyumba zao
moto, kuibiwa chakula kilichokuwa majumbani mwao pamoja na kupotea mifugo
iliokuwa majumbani mwao.
Tatizo hilo lilisababisha kuathiri
shughuli za kiuchumi na kijamii maeneo hayo kutokana na wananchi
kushindwa kufanya shughuli zao kutokana na mapigano hayo kwa kuhofia usalama
wao.
0 comments:
Post a Comment