Pages

Subscribe:

Thursday 23 January 2014

WAZIRI MKUU ANENA KWA WAHANGA WA MAFURIKO DUMILA

WAZIRI mkuu Mizengo amesema kuwa serikali imechukua hatua za dharuala kwa kuhakikisha waathirika wa mafuriko wilayani Kilosa na Mvomero wanapatiwa chakula na dawa huku serikali ikiangalia taratibu zingine za kuwahifadhi waathirika hao katika mahema.
Pinda alisema hayo januari 23 mwaka huu alipotembelea katika eneo la Dumila  na eneo la Magole kuongea na waathirika hao na kujionea hali halisi.
Alisema kuwa tayari serikali kupitia kitengo cha maafa kimeshanza kuchukua hatua za kupeleka chakula  na dawa katika maeneo hayo na kwamba amewahakikishia wananchi walioathirika kuwa watapata chakuala katika kipindi chote ili kuokoa maisha yao.
Hata hivyo waziri huyo alisema kuwa serikali itatumia majeshi yake katika kuhakikisha wananchi hao wanapata makazi ya muda .
‘’ Tunaongea na majeshi ili kuja kutusaidia katika suala la kujenga mahema kwaajili ya maafa haya, wao ndio wataalamu  tunaamini watatusaidia sana.
Alisema kuwa mafuriko hayo ni makubwa sana ambayo yaliwahi kutokea miaka zaidi ya 15 iliopita wilayani Kilosa  mkoani hapa.
Alisema kuwa mafuriko hayo yamekuwa makubwa kutokana na  barabara hiyo ya Morogoro  na Dodoma kuinuliwa  na kuwa kama tuta hali inayosababisha maji kubakia upande mmoja na hivyo kuathiri zaidi.
‘’ Barabara hii ingekuwa kama ilivyokuwa awali maafa yasingekuwa makubwa kama hivi, hivyo kuna kila sababu ya kuangalia jinsi gani watahakikisha wanaondokana na tatizo hilo ‘’ Alisema
Alisema  kuwa serikali imeshaanza kuchukua hatua kupitia kampuni ya ujenzi ya wachina ya wilayani  Kilosa kuweza kujenga daraja hilo ili maroli na magari mengine ambayo yamekwama kuweza kupita na kuendela na safari yake.
‘’ Tumeongea nao wametuahidi watatumia siku nne kujaza mawe ili barabara hiyo iweze kupitika lakini tumewaomba wajitahidi kutumia siku tatu ili kupunguza adha ya wasafirishaji hao’’alisema.
Alisema kuwa kampuni hiyo ya wachina ilishaanza kazi hiyo na kwamba hadi sasa wameshamwaga roli 150 za mawe kwa upande wa Morogoro na wanaendela upande wa Dododma ili kukamilisha kazi hiyo.
Kwa upande wao madereva wa maroli na utigo wao walidai kuwa wanakabiliwa na tatizo la kushindwa kulala kwa kuhofia kuibiwa hivyo kulazimika kukesha wakilinda maroli yao.
‘’ Yaani hapa usiku mzima hatulali tunalala mchana kwani eneo lenyewe sio salama na magari  hayo unayoona zaidi ya 300 tunaogopa kuibiwa ‘’ Alisema Isa Ramadhani mmoja wa utingo wa roli.
Juma Musa mfanyabishara wa mahindi katika eneo hilo la Dumila alisema kuwa kwa sasa biashara imekuwa nzuri kutokana na bidhaa kuuza kwa bei mara mbili ya awali.
Alisema kuwa mahindi ya kuchoma yaliotakiwa kuuzwa shilingi 300 hadi 500 huuzwa kwa shilingi 1000 na ndizi za kuiva zinazouzwa shilingi 100 huuzwa 200 hadi 300.
Nao wananchi wa eneo la Magole walioathirika na mafuriko hayo walidai kuwa vitu vyote vimesomba na maji hivyo hawana mahali pa kulala wala chakula na kwamba tangu jana hawajala kitu.
‘’ Tangu jana tunatabika hatujala kitu, vyakula, mifugo, vyombo vimesmombwa na maji’’ Alisema Mwajuma Omari.
Chama cha Mapinduzi CCm Mkoa wa Morogoro kimesema kuwa  kimepokea taarifa hiyo  ya maafa kwa masikitiko makubwa na kwenda kujionea hali halisi .
Katibu wa CCM mkoa wa Morogoro alisema kuwa wameipongeza serikali kwa hatua za haraka wanazochukua kuwasaidia wananchi hao na kuiomba iendelee kuwasaidia ili kunusuru maisha yao.
Wakati huo huo Waziri mkuu huyo alisema kuwa  Rais  Jakaya Kikwete alituma salama za pole kwa wahanga wa mafuriko hayo na kuahidi kuwa serikali itakuwa bega kwa bega nao katika kipindi hiki ili kuhakikisha wanaokoa maisha ya watu hao na kuona uwezekano wa kuwapatia mahitaji muhimu.
Mwisho

0 comments:

Post a Comment