Pages

Subscribe:

Thursday, 10 April 2014

KAMATI ZAANZA KUWASILISHA TAARIFA ZA BUNGE MAALUM LA KATIBA, WENGI WAPENDEKEZA SERIKALI MBILI

Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba Samuel Sitta akitoa ufafanuzi kwa wajumbe wa Bunge hilo leo mjini Dodoma wakati wa uwasilishaji wa Sura ya Kwanza na Sita wa rasimu ya Katiba mpya.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati namba tano Assumpter Mshama akiwasilisha maoni ya wajumbe wa Kamati yake leo mjini Dodoma juu ya uchambuzi wa sura ya kwanza na sita ya wa rasimu ya Katiba mpya.
Baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wakiwasili leo kwenye ukumbi wa Bunge mjini Dodoma kwa ajili ya kusilikiliza uwasilishaji wa sura ya kwanza na sita ya rasimu ya Katiba mpya.Picha na Bunge Maalum la Katiba.

Na Magreth Kinabo- Dodoma
Baadhi ya Kamati 12 za Bunge Maalum la Katiba leo zimeanza kuwasilisha taarifa zao kuhusu sura ya kwanza nay a sita ya Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Bunge hilo, mjini Dodoma, huku maoni ya walio wengi wapendekeza Serikali Mbili.

Uwasilishaji wa taarifa hizo ulianza mapema leo asubuhi mara baada ya Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta kuanza kikao, ambapo Kamati mbili ndizo zilizopata fursa ya kuwasilisha, kwa mujibu wa muda uliopangwa .Kamati nyingine zitaendelea sasa 10: 00 jioni.

Kamati iliyokuwa ya kwanza kuwasilisha taarifa hiyo ni Kamati namba mbili, ambayo Mwenyekiti wake ni Shamsi Vuai Nahodha , ambaye ndiye aliyeiwasilisha katika Bunge hilo.

Akiwasilisha taarifa hiyo, Nahodha, aliliarifu Bunge hilo, kuwa zipo baadhi ya ibara ambazo hakikuungwa mkono kwa theluthi mbili kwa mujibu wa Kanuni ya 64(1) ya Kanuni za Bunge Maalum la Katiba za mwaka 2014.

Alizitaja ibara hizo ni ibara ya inayohusu “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”, ibara inayohusu “Ukuu na Utii kwa Katiba,” ibara ya 60 inayohusu “Muundo wa Muungano “na ibara ya 61 inayohusu” Vyombo vya Utendaji vya Jamhuri ya Muungano”.

"Kutokana na hali hiyo na kwa kuzingatia kanuni niliyoitaja hapo awali, ibara hizi zinachukuliwa kuwa zimefanyiwa maamuzi, lakini hazikupata theluthi mbili ya upande mmoja. Kwa msingi huo Kamati yangu inazileta ibara hizo pamoja na ibara nyingine mbele ya Bunge hili Maalum ili kufanyiwa maamuzi ya pamoja,” alisema Nahodha.

Akiwakilisha maoni ya walio wengi kuhusu sura ya kwanza ibara ya kwanza(i)inayohusu “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania” alisema wajumbe walikuwa na mjadala maana na maneno ya “Muungano na “Shirikisho”. Hata hivyo katika mjadala huo ufafanuzi kina ulitolewa kuhusu maneno hayo.

Alisema neno Muungano ni makubaliano ya zaidi ya nchi moja kuunda dola moja yenye nguvu ambapo majukumu ya msingi ya nchi hizo yanakabidhiwa kwenye Serikali ya Muungano, wakati Shirikisho ni makubaliano ya nchi mbili au zaidi zinazounda Serikali moja chini ya kiongozi mmoja.

Hivyo baada ya ufafanuzi huo wajumbe walifanya maamuzi katika ibara ya kwanza(1)wajumbe wengi walipendekeza neno shirikisho lifutwe kwa sababu tatu, ambazo kwanza ni hati ya makubaliano ya Muungano inazungumzia kuwepo kwa Serikali mbili yaani Serikali ya Muungano na Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar. Hata Rasimu ya Katiba ibara 1(3) inatambua hati ya Muungano kama msingi na muendelezo wa makubaliano hayo.

Pili hati hiyo ya Muungano mpaka sasa bado haijafutwa na wala haijabadilishwa na tatu Shrikisho la serikali tatu linalopendekezwa katika rasimu , litakuwa dhaifu kiasi cha kushindwa kudhibiti ulinzi wa eneo la bahari ya Hindi lenye rasilimali nyingi ambazo mataifa makubwa wanaziwania.

Aliongeza kuwa udhaifu huo utayapa mwanya mataifa hayo kuzirubuni nchi washirika zisichangie gharama za kuendesha Serikali ya Shirikisho, hasa kwa kuzingatia kuwa Serikali Shirikisho haina vyanzo vya uhakika vya mapato ,hivy endapo jambo hilo likitokea Shirikisho litadhoofika na hatimaye kuvujika.

Aliongeza kuwa katika sura ya sita ibaraya 60 kuhusu Muundo wa Jamhuri ta Muungano wajumbe wengi walikubaliana kuwa Muundo wa Serikali Mbili kama ilivyoanishwa katika hati ya Muungano wa Tanzania, baada ya kupiga kura kwa ajili ya kupata uamuzi ,theluthi mbili upande wa Tanzania Bara haikupatikana. 

Hata hivyo wajumbe wengi walipendekeza ibara hiyo ifanyiwe marekebisho kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakuwa na Serikali mbili ambazo ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Mapinduzi ya Zanzibar. 

Nahodha alisema kwa maoni ya watu wachache , katika sura ya kwanza 1(1) walipendekeza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Shirikisho lenye mamlaka kamili limetokana na Muungano wa Nchi huru mbili za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.

Aidha aliongeza kuwa katika sura ya sita, ibara, 60 hadi 69 zinahusu Muundo wa Serikali walipendekeza zibaki na zisomeke kama zilivyo katika rasimu.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Kamati namba tano (5)ya Bunge hilo, Assumpter Mshama ambayo ilikuwa ya pili kuwasilisha ripoti yake , alisema ibara ya kwanza(1) haikupata theluthi mbili ya wajumbe wote kutoka Tanzania Bara,lakini ilipata theluthi mbili ya wajumbe kutoka Zanzibar.

Aliongeza kuwa ibara ndogo ya (2) na (3) zilipata theluthi mbili ya wajumbe wote kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

Hivyo wajumbe walio wengi kwa kuzingatia Hati ya Makubaliano walipendekeza mfumo wa Serikali Mbili ndiyo unaofaa, ndiyo utakaoimarisha Muungano kama changamoto zilizobainishwa zitatuliwa kisheria na kikatiba.

Assumpter alisema katika sura sita ibara ya 60 ilikataliwa na theluthi mbili ya wajumbe kutoka Tanzania Bara na Zanzibar. Hivyo walipendekeza ibara ya 60 (1) itakuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakuwa na muundo wa Serikali mbili, ambazo ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Alisema maoni ya walio wachache sura ya kwanza ibara ndogo ya kwanza wajumbe walipendekeza kuwa ibaki kama ilivyo lakini irekebishwe kidogo, isomeke Shirikisho la Jamhuri ya Tanzania, ni Shirikisho ambalo limetokana na Muungano wa Nchi mbili za Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.

ibara 1(4) Nchi nyingine yoyote ya Afrika itaweza kujiunga na Shirikisho ili mradi tu inakubaliana na masharti ya Katiba hii.”

Alisema sababu walizozitaja ni Muungano wa Tanzania umetokana na Jamhuri ya mbili kuungana kwa hiari, jina la awali lililotajwa katika Mkataba wa Muungano lilikuwa ni Jamhuri ya Muungano wa Tangayika na Zanzibar.Jina hili lilibailishwa na kuitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika taarifa za kamati hizo, baadhi ya ibara zilifanyiwa marekebisho na nyingine zibaki kama zilivyo.

0 comments:

Post a Comment