Pages

Subscribe:

Wednesday, 23 April 2014

VIJANA WATAKIWA KUJITOKEZA MBIO ZA WAZALENDO

Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa Sixtus Mapunda akiwa na Omar Said Ng'wanang'waka Mkuu wa Utawala UVCCMKatibu Mkuu wa UVCCM Taifa Sixtus Mapunda akiwzungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kushoto ni Omar Said Ng’wanang’waka Mkuu wa Utawala UVCCM
Frank Mvungi-Maelezo
VIJANA wametakiwa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mbio za wazalendo zitakazofanyika Ijumaa wiki hii ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya  miaka 50 ya muungano  wa Tanganyika na Zanzibar.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi  (UVCCM) Sixtus Mapunda wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam.
Mapunda alisema mbio hizo zitaanzia Ofisi ya CCM Vijana, Kinondoni hadi ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere uliopo Posta jijini Dar es Salaam.
Alisema kuwa lengo la mbio hizo ni kuwahamasisha vijana kuweka mbele uzalendo na maslahi mapana ya Taifa hasa katika kipindi hiki cha Maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano.

Aliongeza kuwa vijana wanao wajibu mkubwa wa kuuenzi, kuulinda na kuudumisha  Muungano ili kutimiza jukumu lao katika kipindi hiki Taifa linapofanya mchakato wa kupata katiba mpya.
“Ni wakati muafaka sasa vijana kuonyesha hilo kwa kushiriki katika mbio hizo zinazolenga kuenzi na kudumisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar”, alisema Mapunda.
Alisema kuwa kwa sasa vijana wanatakiwa watumie fursa zilizopo katika maeneo yao katika kujiletea maendeleo kwa kuwa nchi  yetu imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi ambazo zikitumika vyema zitawakomboa vijana”, alisema Mapunda.
Katika kutumia fursa zilizopo hapa nchini Mapunda amesema ni vyema vijana wakajiunga katika vikundi vya uzalishaji mali na hivyo kuweza kunufaika na fursa zilizopo kupitia umoja wao.
Mapunda aliwaasa vijana kuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ndicho kitu pekee kinacholiunganisha Taifa hivyo vijana wana wajibu wa kutimiza lengo hilo.

0 comments:

Post a Comment