Wakazi wa doma wilayani Mvomero wakiwa mbaroni kwa tuhuma za kufunga barabara ya Morogoro na Iringa wakishinikiza wafugaji kuondolewa eneo hilo.
WATU 48 wanashikiliwa na polisi mkoani hapa kwa tuhuma za
kufunga barabara ya Morogoro na Iringa wakishinikiza wafugaji wa jamii ya
Kimasai kuhamisha katika eneo la Doma wilayani Mvomero.
Kamanda wa polisi mkoani hapa Faustine Shilogile alisema
kuwa tukio hilo limetokea Februari 6 mwaka huu majira ya saa 3 asubuhi.
Kamanda huyo alisema kuwa katika tukio hilo walifanikiwa
kuwatia mbaroni wanawake 24 na wanaume 24 ambao wanadaiwa kufanya vurugu hizo.
Alisema kuwa fujo hizo zilitokea baada ya watu hao kudai kuwa
wafugaji hao waliwapiga na fimbo wananchi wenzao waliokwenda porini kukata mkaa
jambo lililowafanya nao kuamua kufunga barabara hiyo.
Hata hivyo kamanda huyo alisema kuwa walifanikiwa kufungua
barabara hiyo majira ya saa 7 mchana baada ya kupiga mabomu ya mchozi kwa lengo
la kuwatawanya wananchi hao.
Alisema kuwa hakuna madhara yeyote ya kibinadamu yaliotokea
ingawa watu hao walijaribu kuwapiga mawe polisi hao .
Alisema kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria na kwamba
watu hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kesho ili kuweza kujibu tuhuma
hizo.
Kwa upande wao wananchi hao wamalalamikia wafugaji hao
kitendo chao cha kuingiza mifugo mashambani na kuharibu mazao njambo ambalo
linawarudisha nyuma kimaendeleo.
Pia walilalamikia uongozi wa kijiji hicho cha Doma kwa
kuwaingiza wafugaji kinyemela hali inayofanya kuwa wengi huku eneo la malisho
likiwa dogo hali inayofanya wafugaji hao kuingiza mifugo yao mashambani.
Ibrahim Ndegalo alisema kuwa mbali na wafugaji hao kuwapiga
lakini pia wamakuwa wakiwanyang’anya mali zao bila sabababu na kwamba maisha
yao yamekuwa hayana amani.
0 comments:
Post a Comment